Saturday, 17 March 2018

W WAPO Social Media

MJUE MUNGU UNAYEMWABUDU-3

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Leo tunaendelea na sehemu ya tatu ya mada hii ya “kumjua Mungu unayemwabudu." Makala mbili zilizotangulia zilijikita zaidi katika tafsiri kuhusu Mungu jinsi alivyojitambulisha kwetu katika maandiko matakatifu. Katika makala ya leo tunakwenda kupitia tafsiri ya misamiati ya kuabudu na sifa stahiki katika kuabudu.

MAANA YA KUABUDU NA VIASHIRIA VYAKE

Katika Biblia takatifu, misamiati ya maneno “kuabudu” au “ibada” yametajwa kwa lugha mbili kuu ambazo ni kiebrania na kiyunani. Neno la kiebrania ambalo ni SHACHAH limetajwa mara 94 limetafsiriwa kuwa ni “kuabudu” ambako maana yake hasa ni “kuinama chini”, au “kusujudia”.

Mfano wa matumizi ya neno SHACHAH tunausoma katika kitabu cha Kutoka kama ilivyoandikwa: “Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.” (Kut.4:31) Neno "kuabudu" katika lugha ya kiyunani ni “PROSKUNEO” na limetajwa 59 katika Agano Jipya likiwa na maana ya “kubusu mkono” na “kuinama chini na kubusu ardhi”.

Katika lugha ya Kingereza kuna maneno matatu yaliyotumika kutafsiri neno “kuabudu”. Maneno hayo ni “honor”, “reverence” na “homage”. Msamiati wa neno “honor” maana yake ni “heshima, tuza, adhama, taadhima, tukuza”; Msamiati wa neno reverence maana yake ni “kicho/uchaji” ambayo ni hali ya “kuogopa”, “hofu”, na “nyenyekea”; na msamiati wa neno homage maana yake ni “heshima kuu na maalum zitolewazo hadharani”.

Kwa kifupi, “kuabudu” maana yake ni “kutoa heshima ya hali ya juu iliyojaa kicho na unyenyekevu inayotolewa kwa ajili ya kumtukuza au kumwadhimisha, Mungu Muumbaji” Katika kuonesha heshima hiyo ndipo hufanyika matendo ya kuabudu ambayo ni pamoja na kupiga magoti, kuinama, kusujudia, kama viashiria vya kuabudu.

Tafsiri nyingine ya maana ya “kuabudu” ni “kutumika”! Kuabudu kunakamilishwa na kumtumikia yule unayemwabudu. Kutumika ni pamoja na kutii na kutekeleza kwa vitendo amri na maagizo ya Mungu. Katika amri za Mungu kuna “maelekezo” na “makatazo” mbali mbali. Mtu anapojitoa mhanga kutekeleza maelekezo na kuzingatia makatazo ya Mungu kwake hayo ni matendo ya kuabudu kwa Mungu.

JIHADHARI NA KUABUDU AMBAKO NI BATILI

Japokuwa watu wengi wanaabudu kupitia dini na madhehebu yake, na kila ibada inatakiwa kuheshimiwa na watu wote, hii haina maana ya kwamba ibada zote zinakubaliwa na Mungu. Sio kila kuabudu kuna kibali mbele za Mungu. Hata kama wenye kuabudu watafanya matendo ya kuabudu kwa juhudi lakini kama wao binafsi hawajakidhi vigezo vya kuabudu alivyoviweka Mungu mwenyewe, basi kuabudu huko ni batili mbele za Mungu.

Unaweza kuhoji ni kwa jinsi gani kuabudu kunakofanywa kwa vitendo vyote vya kusujudia na kuinama na kupiga magoti ati matendo hayo yawe ni batili mbele za Mungu? Ili kujibu swali hili, naombe turejee maneno ya Yesu mwenyewe pale aliposema kwa wayahudi:

“Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yailiyo maagizo ya wanadamu.” (MT.15:8-9)

Maandiko haya yanaashiria kwamba si kila kuabudu ni kamili. Mafarisayo walizingatia matendo ya ibada kwa jinsi ya kuonekana kimwili. Walikuwa wakisifu na kuimba na kusujudia tena kwa bidii. Lakini Yesu anasema pamoja na kuyafanya yote hayo, “mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu” wanayemwabudu. Na kwa sababu hiyo ibada zao zilikuwa ni batili mbele za Mungu!

MSINGI WA KUABUDU NI UCHAJI MUNGU

Tafsiri ya msamiati wa neno “uchaji” kwa kiebrania ni YARE likimaanisha “hofu yenye kuheshimu kwa hali ya juu. Mahali ambalo limetumika ni katika Zaburi kama ilivyoandikwa: “Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.” (Zab.89:7)

Neno jingine la kiebrania linatotafsiri “uchaji” ni SHACHAH ambalo limetumika mara 172 katika maandiko. Maana yake ni “kuinama achini, kuanguka kifudifudi, na kujishusha kwa unyenyekevu"

Katika Agano jipya ambalo lugha ya asili ni kiyunani, neno lililotafsiri “uchaji” ni PHOBEO ambalo maana yake ni “kuogopa, kumwogopa mwingine, kufanya jambo kwa hofu ya kuumizwa, kuchukulia kwa hofu ya utii“ Mojawapo ya maandiko yaliyotumika kutafsiri “uchaji” ni kama ilivyoandikwa katika Mathayo: “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” (Mt.10:28)

Watu wengi hufikiri kuwa na bidii ya kuhudhiria kwenye makusanyiko ya ibada na kusali kwa mbwembwe ndiyo ibada inayompendeza Mungu. Na wengine wametafsiri ibada kuwa ni mahali pa kwenda kupunguza madhambi na wakirudi waanze upya katika maovu yao yale yale. Mtunga Mithali aliandika akisema: “Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.” (Mith.1:7)

Andiko hili limetaja habari za kudharau “hekima” na “adabu” kama viashiria vya kutokumcha Mungu. Kutokumcha Mungu kunadhihirika katika “ukosefu wa adabu” na “utovu wa nidhamu” iwe ni kwa maneno au matendo. Ndiyo maana wahusika wametajwa kuwa ni “wapumbavu” ambao tafsiri yake kibiblia ni watu wasiojali wala kuogopa kumkosea Mungu kwa sababu hata hawatambui uwepo wake. (ZAB.14:1; 53:1)

Kuna watu wengi wenye kudai ni "wakereketwa" wa elimu ya Mungu, na "watetezi" wa imani kuhusu Mungu. Lakini jinsi wanavyojitambulisha na kuwasilisha hoja zao, utadhani huyu Mungu ni babu yao! Kauli zao zimejaa dharau, kejeli, kiburi, na jeuri. Hawana adabu wala heshima mbele za watu wazima waliowazidi umri au wazee wao, wala viongozi na wenye mamlaka juu yao, lakini kisingizio cha kutetea imani na itikadi zao zi kidini hutoa maneno yasiyo na adabu wala hekima mbele za watu na Mungu.

Hata mtume Paulo siku moja alijikutana kwenye kibano cha kujitetea akatamka maneno mahumu kwa kiongozi wa imani alipohojiwa aliomba radhi akisema: “Paulo akasema, sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.” (Mdo.23:5).

Kila mwenye kumcha Mungu lazima atajaliwa hekima na adabu ikiwa ni pamoja na kujizuia kufanya vitendo vyenye kumuudhi Mungu. Mfano hai katika Biblia tunaupata kwa Yusufu mtoto wa Yakobo ambaye alilapolazishwa kuzini na mke wa bwana wake yeye akamkatalia.

Yusufu alikataa kuzini na yule mama sio kwa “hofu ya kufumaniwa”! na bwana wake! Yusufu aliogopa kuzini kwa sababu hii:“…nifanye ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?” (Mw.39:9b). Unaona? kilichomzuia Yusufu asizini ni “kuogopa kukosea Mungu..”! Na hii ndiyo tafsiri ya “uchaji” Mungu ambayo ndio msingi wa kuabudu.

Katika kujumuisha tafsiri ya msamiati wa uchaji maana yake kamili ni “tabia ya kumpa Mungu heshima ya hali ya juu anayostahili; kuogopa kumuudhi na kumkosea Mungu; na pia kumtii Mungu ili kuepukana na ghadhabu yake kwa waasi."

Kusema kweli, kumcha Mungu ndio msingi kamili wa kuabudu. Inawezekana kufanya matendo ya kuabudu pasipo kumcha Mungu na ikawa ni ibada batili. Lakini haiwezekani kumcha Mungu kusiambatane na ibada yenye kibali mbele za Mungu.

Mwenzangu wewe uko upande gani? Je! Unafanya ibada zako kwa kusukumwa na uchaji Mungu; au unamwabudu Mungu kwa nje tu, lakini moyo wako uko mbali naye kitabia na mwenendo? Kwa maelezo zaidi tukutane kwenye madai inayofuata ambayo nitawasilisha “tofauti kati ya mitindo ya ibada za Agano la Kale na ibada za Agano jipya.”

Kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like post hii na tafadhali warushie marafiki zako pia. Ubarikiwe sana!

LATEST VIDEOS

Newsletter

Subscribe to Wapo Mission International weekly Newsletter.

Do you need JESUS as your personal savior?
If YES then Click HERE
Please rate our website

Need To Reach Us?

Email:

info@wapo.or.tz

Phone:

|+255 766 777 126 |
|+255 713 649 865 |
|+255 712 249 724 |
Do you need JESUS? Click here

Who's Online

We have 17 guests and no members online